Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dokta Donan Mmbando, amepongeza ushirikiano wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Benki ya NMB na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kufanikisha Hafla ya kuwazawadia Wanafunzi na Walimu Bora wa Masomo ya Kemia na Biolojia kwa kidato cha Nne mwaka 2013 na Kidato cha Sita 2014.
Katibu Mkuu aliyasema hayo kwenye utoaji wa zawadi hizo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni kutoka taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali na Binafsi, wanafunzi, walimu, wazazi, waandishi wa Habari na watumishi wa Wakala ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Wizara inasisitiza ushirikiano na Sekta binafsi katika kuharakisha utekelezaji wa Sera yake kulingana na Sera ya Ushirikiano baina ya Serikali na Sekta Binafsi (Public Private Partnership) ya mwaka 2009. Nimefurahi kusikia kuwa Wakala umeshirikiana na NMB na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kuwezesha zoezi hili lenye manufaa kwa jamii.”
Kwa kuongezea katika hilo, Katibu Mkuu, alitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza katika kuwezesha zoezi hili la kila mwaka, “Nawapongeza sana wadau wote waliouona umuhimu huu, na kwa fursa hii, nawaomba wadau wengine kuunga mkono kwa kushiriki kwa namna yeyote wanayoona inafaa na wanayoimudu.”
Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel V. Manyele, akiongea kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, alisema Benki ya NMB na Chuo Kikuu Huria wameamua kuunga mkono juhudi hizo baada ya kuona ni jambo zuri linalofanywa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, na pia kuomba taasisi nyingine za Serikali na Binafsi kujitokeza kuwaunga mkono kwa miaka inayokuja.
“Tumeshirikiana na wenzetu wa Benki ya NMB na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mwaka huu, ambao baada ya kuona juhudi zetu, wametuunga mkono. Benki ya NMB wao wametoa zawadi ya pesa taslimu kwa kila mshindi wa kwanza na walimu wote wanne, na Chuo Kikuu Huria wametoa zawadi ya mafunzo ya wiki tano ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa walimu wote wanne na wanafunzi washindi wa kwanza wa kidato cha Nne mwaka 2013 kwa masomo yote ya Kemia na Biolojia.”
Naye Meneja Mwandamizi wa Benki ya NMB upande wa Taasisi, Bi. Noelina Kivaria, alisema kwa miaka kadhaa sasa Benki ya NMB katika mipango yake imekuwa ikishiriki shughuli mbali mbali za kijamii, kama kusaidia sekta ya Elimu na Afya na kufariji jamii kipindi cha majanga kwa sababu wanatambua kuwa huko ndiko ambako wateja wao wengi wanakotoka.
“Kwa miaka kadhaa sasa, NMB katika mipango yake imekuwa ikishiriki shughuli mbali mbali za kijamii, kama kusaidia sekta ya elimu(madawati na viti), afya (vitanda, magodoro na mashuka) na pia kufariji jamii nyakati za majanga kama mafuriko na ajali mbalimbali zinazogusa maisha ya watu wengi.
Tunatambua kuwa ni katika jamii ndiko wateja wetu wengi wanakotoka, kwa hiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni wetu. kwenye sherehe hii, NMB tumeamua kushiriki katika kutoa tuzo kwa wanafunzi 8 (wavulana wane na wasichana wane) waliofanya vizuri zaidi kwenye masomo ya kemia na biolojia.
Hatuishii hapo tu kwani tunaamini kwamba ili mwanafunzi afanye vizuri, mwalimu ana nafasi kubwa sana kuwezesha mafanikio ya mwanafunzi, hivyo basi pia tunawapa tuzo walimu 4 waliowezesha wanafunzi hawa kuwa vinara kwenye Biolojia na Kemia.”
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Tekinolojia ya Kujifunzia na Menejimenti ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk. Edephonce Nfuka, alisema wamevutiwa kushirikiana na Wakala pamoja na Benki ya NMB kuwazawadia wanafunzi hao na walimu kwa kutoa ufadhili wa kozi ya muda mfupi ya TEHAMA yenye ujasiriamali ndani yake kwa wanafunzi wane na walimu.
“Kwa niaba ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Kupitia Taasisi ya Tekinolojia za kujifunzia na menejimenti tunayo furaha kubwa kuungana na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na NMB ili kuchangia katika kuwapongeza kwa kutoa ufadhili kwa walimu wote 4 pamoja na wanafunzi wanne ( Wasichana 2 na Wavulana 2) waliofanya vizuri zaidi katika masomo ya Kemia na Biolojia katika kidato cha nne kuja Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kusoma kozi fupi ya Tehama yenye ujasiliamali ndani yake ( ICT with entrepreneurship) ambayo Chuo kinaitoa kwa kushirikiana na taasisi ya Cisco Academy ya Marekani.
Hii ni kozi fupi inayotolewa na kutambulika kimataifa. Kozi hii itatolewa kwa muda wa wiki 5 na mnaweza kusoma katika tawi lolote la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania lililopo karibu nanyi”
Katika hafla hiyo mbali na wanafunzi, walimu, wazazi na watumishi wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, pia ilihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka wizara ya Elimu, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Bohari ya Madawa (MSD), Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
| ||
No comments:
Post a Comment